Header Ads

Mwenge wamtia matatani Mkurugenzi

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amempa siku mbili Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Kazimbaya Makwega kuhakikisha anawasilisha taarifa ya ujenzi wa darasa la shule ya Msingi Mkundiambaru.
Agizo hilo amelitoa leo Jumanne katika Uwanja wa Ndege wa Tanga baada ya kiongozi wa mbio za Mwenge, Amour Hamad Amour kueleza kwamba akiwa wilayani Lushoto Septemba 22 mwaka huu aligoma kuzindua darasa hilo kutokana na kuwepo dosari ikiwepo kujengwa chini ya kiwango.
Kiongozi wa mbio za mwenge,  Amour amesema “Hadi leo tumepita mikoa 26, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ndiye aliyetukwaza, tulimwagiza kabla hatujatoka Tanga awe ameleta taarifa ya darasa hilo lakini hadi sasa Oktoba 3 hatujamuona. Tunakuomba RC mweleze kuwa awe ameleta taarifa hizo ndani ya siku nne tutakazokuwa Pemba,” amesema Amour.
 Ameongeza kwamba “Tukiwa Lushoto nilimwagiza kabla ya kuondoka Tanga leo awe ameniletea mchanganuo wa makadirio ya kazi na hati ya ununuzi wa vifaa vya mradi lakini  hajaleta. , nampa siku nne awe ametuletea Pemba ili tuweze kupeleka taarifa kwa viongozi wetu waliotuagiza kazi,"
Aidha kiongozi huyo wa mbio za mwenge hakusita kuweleze sababu na dosari alizoziona mpaka kupelekea kukataa kuzindua darasa ni pamoja na darasa dogo lisilokidhi vigezo, lina nyufa na limeezekwa kwa mabati ya geji 32 badala ya 28.
Mkuu wa mkoa, Shigella amesema atahakikisha taarifa hiyo inawasilishwa kwa kiongozi huyo kesho Jumatano. “Wewe umetoa siku nne, mimi namwagiza kesho awe ameshawasilisha taarifa hiyo,” amesema Shigella

No comments