Mbinu za kumkamata dereva wa Lissu
Familia ya Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha wanasheria
Tundu Lissu, imemshauri Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro kuchukua
hatua za kumfuata dereva wa Lissu, Jijini Nairobi na siyo kumuita aje
kwa ajili ya Mahojiano
Wakizungumza
leo na wanahabari, Kaka wa Tundu Lissu ambaye pia ni Wakili, Alute
Mughwai Lissu amesema kwamba, Jeshi la polisi kama wameona kwamba dereva
wa Lissu anaweza kuwa msaada kwa ajili ya upelelezi wao basi watumie
ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Kenya kufanya naye mahojiano na
dereva huyo.
Mughwai amesema kwamba kitendo cha kukaa
kwa takribani mwezi mzima kwa ajili ya kumsubiri Dereva wa Lissu
wangekuwa wameshakwenda Nairobi na wakawa wameshapata maelezo
wanayohitaji.
"Siku zote dereva yupo
hospitalini anamuuguza bosi wake. Wakamchukue pale waende nao kwenye
ofisi za Ubalozi na wachukue maelezo badala ya kusubiri. Katika tukio la
shambulio la Lissu kama dereva angekufa inamaana wangeacha upelelezi si
wangeeendelea? Basi wafanye upelelezi kwa njia hiyo na siyo kumuita
arudi nchini ili kumhoji". Mughwai
Mughwai amehoji kwamba "Mpaka
sasa kama watu hawajakamatwa, je wanamuhakikishiaje usalama dereva
huyo, isije akatoka huko kuja kuhojiwa alafu akiwa anapita Namanga
anakuja anakatishwa usalama wake njiani. Na kama wataenda kumchukua
busara inaeleza kwamba aweze kuhifadhiwa ahakakikishiwe usalama wake,
achukuliwe maelezo na ahifadhiwe siyo jela kwani yule ni shahidi tu.
Ameongeza kwamba wao kama famillia
hawana maslahi na chama chochote na hawako tayari kuona jambo la
shambulio la ndugu yao likafanywa siasa bali wanachotaka ni shambulio
hilo liweze kufanyiwa uchunguzi pamoja na ndugu yao kupona.
Hata hivyo mdogo wa Tundu Lissu Vicenti
Mugwai amewashukuru Watanzania wanaofanya maombi kwa Lissu pamoja
kuendelea kuwatolea michango kwa ajili ya matibabu ya ndugu yao
Tundu Lissu alipigwa risasi zaidi ya 30
katika gari lake na zaidi ya tano inadaiwa kumpata mwilini mwake mnamo
Septemba 7 , 2017 majira ya mchana nje ya makazi yake Area D Dodoma.
Post a Comment