Mkuu wa wilaya atoa siku saba
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Saum Hapi amemjia juu mwekezaji Liu
Deng Wei na kumpa siku saba kuhakikisha analipa stahiki zote za
wafanyakazi.
Hayo yametokea leo baada ya Mkuu huyo wa
Wilaya kufanya ziara katika Mgahawa wa Tangren uliopo Mikocheni jijini
Dar es Salaam ambapo amekutana na mwekezaji anayemiliki mgahawa huo
pamoja na wafanyakazi ambao wameeleza kuwa na malimbikizo ya malipo yao.
Wafanyakazi wameeleza kutolipwa
malimbikizo yao kwa muda wa miaka kumi ikiwemo kufanya kazi bila likizo
pamoja na kutopewa malipo ya kufanya kazi kwa muda wa ziada ‘Over Time’.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo DC
Hapi ameagiza stahiki zao zishughulikiwe ndani ya siku saba. Pia Hapi
ameagiza wafanyakazi waunganishwe kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii
haraka iwezekanavyo na wapewe mafunzo ya namna inavyofanya kazi.
"Tunapenda
sana wawekezaji lakini sio wawekezaji wasiofuata misingi, taratibu na
sheria za nchi, namuomba mwekezaji alipe malimbikizo yote ya wafanyakazi
na awaunganishe na mifuko ya hifadhi za jamii vinginevyo tutachukua
hatua zaidi", Amesema DC Hapi.
Pia DC Hapi katika ziara yake
ametembelea kiwanda cha kutengeneza lifti cha SEC East African kilichopo
Masaki na kuutaka uongozi wa kampuni hiyo kuweka mahusiano mazuri na
wafanyakazi wao ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Post a Comment