Idadi ya waliokufa kwa gongo yaongezeka
Idadi ya watu waliofariki kwa kunywa pombe aina ya gongo jijini Dar es
salaam katika eneo la Kimara, imeongezeka na kufikia 10 mpaka sasa.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa polisi kanda maalum Dar es salaam,
Lazaro Mambosasa, amesema tukio hilo limetokea Oktoba 3, 2017 eneo la
Kimara Stop Over kwa mama Anoza, ambaye ndiye alikuwa akiuza pombe hiyo.
Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kusema kwamba walipata taarifa
kutoka kwa watu tofauti ambao ni miongoni mwa ndugu wa marehemu, kuwa
ndugu yao alikunywa pombe kwa mama Anoza na kuanza kupata maumivu ya
tumbo, kisha baadaye kufariki dunia.
”Tulipokea taarifa kutoka kwa mwananchi aitwaye Matigo Ramadhani
mkazi wa Stop Over, kwamba ndugu yake alikwenda kunywa pombe kwa mama
Anoza, aliporudi akawa analalamika maumivu ya tumbo, akampeleka
hospitali ya Mwananyamala na kutibiwa kisha akarudishwa nyumbani, baada
ya muda mfupi akafariki dunia”, amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa ameendelea kusema kwamba ...”Baada ya muda alitokea
mtu mwengine kuja kuripoti kuwa aliporudi nyumbani hakumkuta
mlinzi wake ajulikanaye kwa jina la Yona, na baada ya kumtafuta
walimkuta akiwa amefariki nje ya uzio”, amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema miili mingine ya watu 8 imehifadhiwa katika
hospitali ya Tumbi Kibaha, huku polisi wakiendelea kumtafuta mwanamke
huyo (Mama Anoza) ambaye hajulikani aliko mpaka sasa, na badhi ya pombe
imeshachukuliwa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali ili kubaini nini
hasa chanzo cha vifo hivyo.
Post a Comment