Hatimaye Malinzi na wenzake kuhojiwa na TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa mara ya pili, kumhoji aliyekuwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa.
Jamal Malinzi
Ombi hilo limewasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali wa TAKUKURU, Leornad Swai mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, baada ya shahidi wa 11 katika kesi hiyo kumaliza kutoa ushahidi wake.
Swai amedai kuwa Januari 16, 2019 waliomba kuwahoji washtakiwa hao, lakini hawakuweza kwa sababu walitoa sababu zao kuwa wahojiwe siku nyingine.
Baada ya Swai kumaliza kuwasilisha, hakimu Kasonde alikubaliana na ombi hilo na kutoa ruhusa kwa TAKUKURU kuwachukua kwa ajili ya mahojiano.
Hakimu Kasonde alisema washtakiwa hao watahojiwa Machi 8, 2019 na kesi itaendelea kusikilizwa Machi 19,2019.
Mbali ya Malinzi na Mwesigwa, mshtakiwa mwingine ni Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga, Meneja wa ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na Karani Flora Rauya, ambapo wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni dola za Kimarekani 375,418 ambazo ni takribani sh millioni 882.6 za kitanzania.
Post a Comment