Mwendokasi waua wawili
Watu
wawili wamefariki dunia baada ya lori lililokua limepakia makaa ya mawe
mali ya kampuni ya Full Cargo Support kupinduka katika eneo la Utwango
wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma likitokea wilaya ya Mbinga mkoani humo
kuelekea jijini Dar es salaam.
Kamanda
wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, SACP Gemini Mushy amewataja watu hao kuwa
ni Ahmad Rajab (47) aliyekuwa dereva wa lori hilo pamoja na Abiud Daudi
(25) aliyekuwa utingo wa lori hilo na amesema chanzo cha ajali hiyo ni
kutokana na mwendokasi wa dereva wa gari hilo iliyopelekea kushindwa
kumudu kona ya barabara hiyo na hatimaye kuacha njia na kupinduka eneo
la mtoni na kisha kupelekea vifo vyao papo hapo.
Kwa mujibu wa kituo cha Televisheni ya ITV imesema kuwa imeshuhudia
shughuli za uokoaji wa miili ya watu hao zikiendelea kutokana na kubanwa
vibaya na vyuma vya lori hilo aina ya Daf lenye namba za usajili T 782
CMC na tela T 841 CLP mali ya kampuni ya Full Cargo Sapport mara baada
ya gari hilo kuacha njia na kupindukia katika eneo hilo la Utwango
wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma leo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Utwango wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Bw.
Optatus Mapunda amesema eneo hilo limekuwa likisababisha ajali mara kwa
mara na kwamba mwezi uliopita lori mali ya Dangote likiwa limepakia
makaa ya mawe nalo lilipinduka.
Post a Comment